Tambwe aishika Yanga pabaya



SHIRIKISHO la Soka Duniani FIFA, limewapiga nyundo klabu ya Yanga kutosajili ndani ya vipindi vitatu mfululizo, ikiwa ni baada ya aliyekuwa mchezaji wa klabu hiyo Amis Tambwe kushinda kesi dhidi yao. Usajili huo unadaiwa utahusisha wachezaji wa kigeni tu.
Tambwe aliitumikia Yanga kwa kujitolea akitokea kwa watani zao Simba ambao walimfungashia virago dakika chache dirisha la usajili kufungwa misimu kadhaa iliyopita.
Kwa mujibu wa Wakili wa Tambwe Felix Majani, FIFA imefikia hatua hiyo baada ya Yanga kuonekana kukaidi amri ya kumlipa mchezaji huyo zaidi ya Sh 40milioni ikiwa ni sehemu ya usajili wake sambamba na mishahara yake.
"Tambwe anaidai Yanga tangu atoke mwaka 2019, tukapeleka kesi FIFA na mteja wangu akashinda na FIFA wametoa uamuzi na sasa ni utekelezaji tu," alisema na kuongeza kama muda huo utapita bila Yanga kulipa wataanza kupoteza pointi katika mechi zake za ligi.
"Sasa tunawasubiri wao Yanga kama wanahitaji kusajili hapo wanatakiwa walitatue wao kwa kulipa fedha hizo ili adhabu itenguke, vinginevyo hawatasajili na muda ukipita watapokwa pointi," amesema Majani.
Naye Tambwe alipoulizwa alisema kwa kifupi; "Mimi nilikuwa nimelala wakili wangu kanitumia barua kutoka FIFA kuwa Yanga, wamefungiwa kusajili vipindi vitatu kwa maana ya usajili mkuu, na dirisha dogo pamoja na usajili Mkuu 2022 hawatasajili, bado hawanilipa kama amri ya FIFA ilivyotaka," amesema Tambwe.
Kwa upande wake Afisa Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amesema, hawana shaka na suala hilo, hakuna haja ya kujenga shaka ya mil 40 wakati wamelipa pesa nyingi za madeni.
"Nawaondoa shaka mashabiki wa Yanga hili suala limeisha kwa chapa GSM hakuna kinachoharibika, GSM kalipa madeni millioni 500 sasa hiyo 40 mbona ndogo kabisa," Nugaz amesisitiza.

Post a Comment

0 Comments